KISWAHILI KIDATO CHA TATU ,MADA YA PILI: MJENGO WA TUNGO


                    TUNGO

Tungo ni kipashio cha kisarufi kilichoundwa kwa kuunganisha pamoja vipashio vidogovidogo vilivyo chini yake. 

Au tungo ni neno au kikundi cha maneno ambacho hudokeza taarifa fulani ambayo huweza kuwa kamili au isiyo kamili.

Kwa maana hii, tungo hujengwa na vipashio vidogovidogo kama vile mofimu kuunda neno, neno kuunda kirai, kirai kunda kishazi na kishazi kuunda sentensi. Kama tulivyokwisha kuona hapo juu tungo huanzia neno; rejea aina za tungo.

          AINA ZA TUNGO

Tungo neno: Tungo neno ni tungo ambayo huundwa na vipashio vidogo zaidi ya neno ambayo ni mofimu au fonimu. Mfano;  anacheza, kakimbia.

Tungo Kirai: ni kipashio cha kimuundo chenye neno moja au zaidi lakini ambacho hakina muundo wa kiima kiarifu. Mfano; mtoto mzuri, kiyama chake, bondeni

Tungo kishazi:Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.

KIRAI NA UAINISHAJI WAKE

Dhana ya kirai itaeleweka vizuri kwa kuzingatia sifa zake zifuatazo:

Kirai  ni kipashio cha kimuundo kisichokamilika; yaani ni kipashio kisichokuwa na muundo wa kiima – kiarifu kama zilivyo sentensi ambazo zinahusisha mtendaji wa tendo na tendo linalotendwa.

Kirai huainishwa kimuundo kulingana na neno kuu la kirai husika.

Kirai ni tungo, yaani ni aina moja wapo ya tungo, aina nyingine za tungo ni neno, kishazi na sentensi.

Kirai hudokeza maana, lakini maana hiyo si kamili.

Maneno katika kirai lazima yapangwe kimantiki kwa mpangilio unaokubalika katika sarufi ya lugha husika.

 Japo virai huainishwa kimuundo, huweza kutumika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi.

 Kirai huweza kutokea upande wowote, wa kiima au kiarifu katika sentensi. 

Kirai ni kikubwa kuliko neno
Kama tulivyobainisha hapo juu aina ya virai hukitwa katika aina za maneno ambazo ndizo chimbuko la mahusiano maalumu ndani ya vipashio hivyo.

kirai nomino (kn)
 Ni kirai ambapo neno lake kuu ni nomino. 

Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa kwenye nomino au mahusiano ya nomino na neno au mafungu ya maneno.

KIRAI KITENZI (KT)

 Kirai-kitenzi ni kirai ambacho kimekitwa katika kitenzi au katika mahusiano ya Kitenzi na neno au mafungu mengine ya maneno. Hii ina maana kuwa neno kuu katika aina hii ya virai huwa ni kitenzi.

KIRAI KIVUMISHI (KV)

 Kirai-kivumishi ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika kivumishi. Kwa kawaida muundo huu huwa ni wa kivumishi na neno au fungu la maneno linaloandamana nacho.

KIRAI KIELEZI (KE)
Tofauti na aina nyingine ya virai miundo ya virai vielezi haielekei kukitwa kwenye mahusiano ya lazima baina ya neno kuu (yaani kielezi) na neno au fungu la maneno linaloandamana nalo. Badala yake miuundo inayohusika hapa ni ya maneno ambayo hufanya kazi pamoja katika Lugha kama misemo, neno au maneno yanayofuata neno lililotangulia yakifafanua zaidi neno hilo.
Virai viunganishi (KV)
 Ni kirai ambacho muundo wake umekitwa katika mahusiano baina ya kwa na katika, au kwenye na fungu la maneno linaloandamana nacho. Kwa maneno mengine kirai hicho ni kile ambacho neno kuu ni kiunganishi.

TUNGO KISHAZI
Kishazi ni tungo yenye kitenzi ambacho chaweza kujitosheleza na kukamilisha ujumbe uliokusudiwa na mzungumzaji au kuwa na kitenzi kisichoweza kujitegemea chenyewe.

SIFA ZA KISHAZI
1.Kishazi hupatikana katika/ ndani ya sentensi.

2. Lazima kishazi kiwe na kitenzi, sehemu yoyote ya sentensi isiyo na kitenzi, haiwezi kuwa kishazi. Kishazi huru hutawaliwa na kishazi kikuu na kishazi tegemezi hutawaliwa na kishazi tegemezi.

3.Baadhi ya vishazi huweza kujitegemea kama sentensi hata vikiondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu. Kishazi kinachoweza kujisimamia kama sentensi huitwa kishazi huru kikiwa ndani ya sentensi kuu na huitwa “sentensi sahili” kikiwa sentensi inayojitegemea.

4.Baadhi ya vishazi haviwezi kujitegemea kama sentensi ikiwa vitaondoshwa katika muktadha wa sentensi kuu.

5.Vishazi vingi, hata vishazi huru huwa na kiima dhahiri.

6.Kishazi kwa kawaida, hasa kishazi huru huwa na kitenzi kimoja kikuu.

7. Kitenzi hicho huweza kuandamana na kitenzi kisaidizi. Pia, kitenzi katika kishazi huweza kuwa kitenzi kishirikishi.

8.Kishazi hutekeleza majukumu mbalimbali ya kisarufi.
Tofauti ya kishazi na sentensi ni kwamba kishazi hupatikana ndani ya sentensi lakini sentensi hujisimamia kimuundo na kimaana.
Kishazi huwa na kiarifu kimoja na kiima kimoja, Lakini sentensi huweza kuwa na kiima kimoja.

AINA ZA VISHAZI

1.Vishazi huru

Kishazi huru ni kishazi kinachotaewaliwa ka kitenzi kikuu, ambacho kwa kawaida hutoa ujumbe kamili usiohitaji maelezo zaidi ya kukamilisha maana. Ni kishazi ambacho hata kikiondolewa katika muktadha wa sentensi ambamo vimejikita huweza kujitegemea kama sentensi.

Vishazi tegemezi
Kishazi tegemezi ni kishazi kinachotawaliwa ka kitenzi kisaidizi, ambacho muundo wake hukifanya kutegemea kitenzi cha kishazi huru ili kuweza kutoa ujumbe uliokusudiwa. Kishazi tegemezi peke yake hakitoi ujumbe unaojitosheleza

SIFA ZA KISHAZI TEGEMEZI
1. Kishazi tegegemezi hutoa maana kamili kinapoandamana na kishazi huru.
2. Kishazi tegemezi kinaweza kufutwa katika sentensi bila kuharibu maana ya sentensi nzima.
3. Kishazi tegemezi hutambulishwa na viambishi vya utegemezi
Vinavyoambatanishwa kwenye kitenzi.
4. Kishazi tegemezi vile vile kinaweza kutambuliwa kwa kuwepo vishazi kama vile ingawa, kwamba, ili, kwa sababu, mzizi wa amba, mofu ya masharti n.k

Aina ya vishazi tegemezi

 1.Vishazi tegemezi vivumis.hi
Vishazi tegemezi vinavyotokea pamoja na nomino inayovumishwa.
Vishazi tegemezi visivyoambatana na nomino inayovumishwa

 2.Vishazi tegemezi vielezi
 3.Vishazi tegemezi vya mahali
 4.Vishazi tegemezi vya wakati
5.Vishazi tegemezi vya namna au jinsi
6. Vishazi tegemezi vya masharti
7. Vishazi tegemezi vya hali, hitilafu au kasoro iliyoko katika tendo.
8. Vishazi tegemezi vya sababu/chanzo

Dhima na hadhi ya vishazi

Kishazi chaweza kuwa huru kikajitegemea chenyewe kwa kuwa na maana kamili inayojitosheleza. Lakini kuna vishazi ambavyo havijitoshelezi vyenyewe, bali hutegemea vishazi vingine. 
 Kishazi huru kina hadhi ya sentensi (sahili). Kishazi tegemezi hakina hadhi hii, vishazi tegemezi ambavyo hutegemea vishazi vingine hushuka daraja na kuchukua dhima ya kikundi. 
Baadhi ya vishazi tegemezi huchukua dhima (hufanya kazi) ya kivumishi katika tungo ambayo kwa kawaida ni dhima ya kikundi au neno. Vishazi hivi huvumisha nomino katika tungo hiyo.
UFAFANUZI WA AINA ZA TUNGO
Sentensi
Sentensi ni kifungu cha maneno kuanzia neno moja na kuendelea chenye muundo wa kiima na kiarifu na kinacholeta maana kamili.
Sifa za sentensi
1.Sentensi lazima iwe na mpangilio wa maneno ambao unakubalika na wazungumzaji wa lugha husika.
2.Sentensi lazima ikamilike kimaana, kimuundo na kisarufi.
3.Sentensi huwa na muundo wa kiima na kiarifu /huwa na kirai nomino na kirai kitenzi.
4. Sentensi huweza kuwa na zaidi ya kiima kimoja na kiarifu zaidi ya kimoja.
5.Sentensi inaweza kuundwa na kitenzi kikuu kimoja au zaidi.
6. Sentensi inaweza kuundwa na kishazi huru kimoja au zaidi na kishazi tegemezi kimoja au zaidi.
7. Sentensi huonyesha hali mbalimbali, kama vile amri, ombi, mshangao, swali n.k
Muundo wa sentensi
Muundo wa sentensi kimapokeo/kikazi/kidhima
Muundo wa sentensi kimapokeo/kikazi/kidhima unakuwa na vipengele vifuatavyo:
Kiima: Ni sehemu katika sentensi ambayo hujaza sehemu ya mtenda au mtendwa wa jambo linaloelezwa. Katika tungo kiima hutokea kushoto mwa kitenzi.
Kiarifu: Ni sehemu katika sentensi inayojazwa na maneno yanayo arifu tendo lilofanywa, linapofanywa au litakapofanywa. Kiarifu ndiyo sehemu muhimu zaidi katika sentensi ambayo wakati mwengine huweza kusimama pekee, kwani wakati mwingine huchukua viwakilishi vya kiima.
Vipashio vya kiima
1.Nomino peke yake
2.Nomino, kiunganishi na nomino
3. Nomino na kivumishi
4. Kivumishi na nomino
5. Kiwakilishi peke yake
6.Kiwakilishi na kivumishi
7. Nomino na kishazi tegemezi vumishi
Kitenzi jina
8. Nomino na vivumishi zaidi ya kimoja
9. Kitenzi jina na nomino
Vipashio vya kiarifu
 Kitenzi kikuu peke yake.
 Kitenzi kisaidizi au vitenzi visaidizi vilivyosambamba na kitenzi kikuu.
 Kitenzi kishirikishi na kijalizo
 Yambwa (shamirisho)
 Kijazalio
Chagizo
Sifa za chagizo
Chagizo kwa kawaida huwa ni kielezi au kirai husishi ambacho kinafanya kazi kama kielezi.
Kwa kawaida ni vipashio vya ziada. Si lazima viwepo katika sentensi ili ijisimamie.
Huwa cha lazima ikiwa kinafuata kitenzi kishiriki. Hali ikiwa hivyo, kinafnaya kazi kama kijalizo.
Hutumika kufafanua kitenzi/kivumishi /kielezi.
Hutumika kujaliza kiima/kama kijalizo.
Aina za sentensi
Aina za sentensi kimuundo ni pamoja na hzi zifuatazo
Sentensi sahili
Ni sentensi ambayo huundwa na kishazi huru kimoja. Sentensi ya aina hii huwa inaelezea taarifa moja tu. Mfano; Wanafuzi wanafanya mtihani; Walinzi walitaka kunizuia nisiingie ndani.
Miundo ya sentensi sahili
1. Muundo wa kitenzi kikuu peke yake. Mfano: Gari limeanguka
2.Muundo wa kitenzi kikuu na kitenzi kisaidizi. Mfano: Mgosiyuda alitaka (TS) nisipate (T) utajiri
3.Muundo wa vira-vitenzi vilivyokitwa katika kitenzi ‘kuwa’. Mfano: John amekuwa akiangalia TV kwa muda mrefu sana.
4. Muundo wa kitenzi shirikishi. Mfano: Kiswahili ni tunu ya Taifa
Sifa za sentensi sahili
1.Ina kiima ambacho kimetajwa wazi au kimeachwa kutajwa kwa kuwa kinaeleweka.
Ina kiarifu ambacho kimeundwa na kitenzi kikuu kimoja au kitenzi kikuu na kitenzi kisaidizi au kitenzi kishirikishi na kijalizo na chagizo.
Haifungamani na sentensi nyingine na hivi inajitosheleza kimuundo na kimaana.
Sentensi changamano
Hii ni sentensi yenye kishazi huru kimoja au zaidi na kishazi tegemezi kimoja au zaidi. Sifa moja kubwa ya sentensi changamano ni kuwa na kishazi tegemezi ambacho hutegemea kishazi kingine huru ndani ya sentensi hiyo. Msingi muhimu wa uhusiano ndani ya sentensi hizo ni ule wa kishazi kimoja kutegemea kingine
Sentensi changamano ina muundo wenye vishazi virejeshi. Mfano: Gari liliopinduka jana jioni halikuharibika hatata kidogo.
Sentensi ambatano
Hii ni sentensi inayojengwa na sentensi mbili au zaidi zilizounganishwa kwa kutumia viunganishi kama vile likini, wala, au, na, nakadhalika.
Miundo ya sentensi ambatano
1.Miundo yenye sentensi sahili tu. Mfano: Mwalimu anafundisha wakati wanafunzi wanapiga kelele.
2.Miundo yenye sentensi sahili na changamano. Mfano: Walinzi waliposhindwa polisi waliwasaidia lakini hawakuweza kuwakamata majambazi.
3.Miundo yenye sentensi changamano tu. Mfano: Barabara zilizojengwa na wakoloni zimedumu hadi leo wakati zile zilizojengwa na Wachina hata mwezi hazifikishi.
4.Miundo yenye vishazi visivyounganishwa kwa viunganishi.
Uchanganuzi wa sentensi
Uchanganuzi wa sentensi ni mchakoto unaohusika na kuchanganua vipashio vyote vinavyuonda sentensi kuanzia ngazi ya kategoria ya neno. Katika kipengele hiki utaweza kujifunza hatua muhimu za kuzingatia wakati wa uchanganuzi wa sentensi. Pia utajifunza njia mbalimbali zinazotumika katika uchanganuzi wa sentensi.
Hatua za uchanganuzi wa sentensi
1.Kutaja aina ya sentensi, yaani kama ni sahili, changamano au ambatano.
2. Kutaja sehemu zake kuu, yaani kiima na kiarifu au kirai nomino na kirai kitenzi.
3.Kutaja sehemu kuu za kiima na kiarifu au sehemu kuu za kirai nomino na kirai kitenzi.
4.Kutaja sehemu zote za maneno yaliyomo katika sentensi hiyo.