KISWAHILI KIDATO CHA V---VI
TAFSIRI NA UKALIMANI
Tafsiri [Translation]
Dhana ya Tafsiri.
Tafsiri imefasiliwa kuwa, ni Kutoa mawazo kutoka katika lugha moja kwenda lugha nyingine bila ya kubadilisha maana. [TUKI 2002: 271]
Newmark (1982) Tafsiri ni jaribio la kuwasilisha ujumbe uleule ulioandikwa katika lugha moja kwa lugha nyingine.
Mwansoko na wenzake (2006) Tafsiri ni zoezi la uhauwilishaji wa mawazo katika maandishi kutoka lugha moja hadi lugha nyingine.
Nida na Taber (1969) wanaona kuwa tafsiri hujumuisha upya ujumbe wa lugha chanzi kwa kutumia visawe asilia vya lugha lengwa vinavyokaribiana zaidi na lugha chanzi, kwanza kimaana na pili kimtindo.
Nida na Tiber wanaona kuwa katika tafsiri kitu muhimu ni kuzingatia maana na mtindo. Ukiangalia wataalamu hawa utaona kwamba wanafanana. Wanakubaliana yafuatayo:
(1)Wanaona kuwa tafsiri hufanywa katika maandishi.
(2) Ni lazima kuwe na mchakato wa uhaulishaji.
(3)Ni lazima kuwe na ujumbe unaokusudiwa kupatikana
Kwahiyo kwa fasili ya jumla tunaweza kusema kuwa, kutafsiri ni mchakato wa uhaulishaji wa ujumbe ulio katika maandishi kutoka lugha moja (lugha chanzi) kwenda lugha nyingine (lugha lengwa).
MFASIRI NI NANI?
Ni mtu yeyote anayejishughulisha na kazi za kutafsiri.
Ni mtu mwenye taaluma au ujuzi wa kutafsiri na ambaye anajishughulisha na kazi hizo (weledi-Professionalism)
MATINI NI NINI?
Ni wazo au mfululizo wa mawazo ambao unajitosheleza kimaana.
Matini inaweza kuwa neno moja, kirai, kishazi, sentensi, aya, kifungu cha habari nk. Matini inaweza kuwa ya kimaandishi aua mazungumzo lakini kwa kuwa tunazungumzia tafsiri, tutajadilid matini andishi.
AINA ZA MATINI
Kuna aina mbili za matini ambazo ni Matini Chanzi (MC) na
Matini Lengwa /matini tafsiri.
· Matini Chanzi (MC)
ni matini ambayo iko katika lugha yake ya awali au lugha yake iliyoandikiwa kabla ya mchakato wa kutafsiri.
Matini Lengwa (ML)
ni matini iliyotafsiriwa kutoka lugha yake iliyoandikiwa.
Lugha Chanzi (LC) ni lugha iliyotumika kuandikia matini chanzi (Source language)
Lugha Lengwa (LL) (Target language) ni lugha iliyotumika kutafsiria matini chanzi au lugha unayoitumia kufanyia tafsiri.
KISAWE/USAWE
Katika muktadha wa tafsiri kisawe ni neno, kirai, kishazi, sentensi au hata maneno katika lugha lengwa ambayo maana na matumizi yake yanalingana au kukaribiana na yale ya neno, kirai, kishazi, sentensi au msemo mwingine katika lugha chanzi
DHIMA / UMUHIMU WA TAFSIRI
· Ni njia ya mawasiliano/daraja kati ya watu au jamii mbili zinazotumia lugha tofauti. Mfano; maelezo mbalimbali ya jinsi ya kutumia bidhaa mbalimbali kama vile redio, simu, kurunzi, dawa, jokofu nk.
· Ni nyenzo ya kuelezea utamaduni kutoka jamii moja kwenda jamii nyingine. Mfano; kupitia dini – tafsiri ya Biblia au Kuruani “Koran”, Pia hata katika burudani – tafsiri ya vitabu mbalimbali ambavyo vina vipengele vingi sana vya utamaduni kama vile nyimbo nk.
· Ni mbinu ya kujifunzia au kufundishia lugha kimsamiati na kisarufi.
· Ni kazi ya ajira kama kazi nyingine, hivyo huweza kumpatia mtu kipato.
· Humliwaza mfasiri; hii ni baada ya kumaliza kufasiri.
SIFA ZA MFASIRI BORA
· Awe mahiri wa lugha mbili zinazohusika; kuwa mahiri katika lugha maana yake nini? Ni kujua vizuri nyanja mbalimbali za Isimu ya lugha husika kama vile; Fonolojia-Matamshi, Mofolojia-Maumbo, Sintaksia-Muundo na Semantiki-Maana.
· Ajue vizuri utamaduni wa watu mbalimbali.
· Ajue angalau lugha mbili
· Awe na maarifa ya TEHAMA (ICT)
· Awafahamu watu, jamii na utamaduni wao – mitazamo kuhusu watu, mitazamo – kuhusu wanyama.
. Awe na ujuzi wa kutosha katika uwanja ambao tafsiri anayoifanya imeandikiwa
·Apende kujisomea na kujiendeleza kulingana na mabadiliko ya jamii. Mfano; kusoma vitabu, majarida, magazeti mbalimbali kusikiliza redio na kuangalia TV nk.
· Awe mwandishi bora.
.Awe na weledi na taaluma ya tafsiri
MAADILI YA MFASIRI BORA (ETHICS)
· Awe mwaminifu kwa matini na kwa mwenye matini; yaani asipotoshe habari au kusema uongo.
· Awe mchapakazi (Kujituma/Bidii katika kazi)
· Awe nadhifu – Unadhifu-mwonekano wa moyo, asiwe tapeli/laghai
· Aelewe/kuelewa taratibu za kazi na kuzifuata. Mfano; bei ya kutafsiri kwa ukurasa au kwa maneno.
· Ushirikiano/kushirikiana na watu mbalimbali wa fani mbalimbali, makundi mbalimbali ikiwa pamoja na wafasiri wenzake.
Njia / mbinu za Tafsiri
Zipo njia mbalimbali ambazo hutumika katika kutafsiri, baadhi ya njia hizo ni kama vile:
(i) Tafsiri ya neno kwa neno. [Word to word translation]
(ii) Tafsiri sisisi.[ Literal translation]
(iii) Tafsiri ya kimaana/uwazi.[ Semantic translation]
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano.[Communicative translation]
(i) Tafsiri ya neno kwa neno [Word to word translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha.
Katika aina hii ya tafsiri mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha chanzi hubakia vilevile bila kubadilika. Na kwa kawaida matini inayotafsiriwa huandikwa chini ya matini ya lugha chanzi. Tazama mifano ifuatayo ya tafsiri ya neno kwa neno:
Kiswahili: Alisoma hadi asubuhi
Kingereza: He/past/study/until/morning
Kiswahili: Alikimbia mpaka ofisini kwake
Kingereza: He/past/run/until/office/his
Kiswahili: Anasoma kitabu changu
Kingereza: He/present/book/my
Kiswahili: Walikula chakula chote
Kingereza: They/past/eat/food/all
Umuhimu wa njia hii, humsaidia mtu kuelewa muundo wa lugha chanzi na jinsi lugha chanzi inavyofanya kazi, kaina hii ya tafsiri hutumiwa na wataalamu wa lugha kuonesha namna maumbo au muundo wa lugha chanzi ulivyo, lakini mapungufu yake ni kuwa, aina hii ya tafsiri huwa haitoi maana inayokusudiwa kwa uwazi zaidi.
(ii) Tafsiri sisisi [ Literal translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana za msingi katika lugha chanzi bila kujali sana muktadha lakini ni tafsiri inayofuata mfumo wa kisarufi hasa kipengele cha kisintaksia ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: He was taken at the Central Police Station
Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha police.
Badala ya kuwa: Alipelekwa kituo kikuu cha polisi
(iii) Tafsiri ya kisemantiki/maana au uwazi [Semantic Translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi. Katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa kufuata sarufi hususani vipengele vya kisemantiki na kisintaksia ya lugha chanzi. Inaitwa tafsiri ya kisemantiki kwa sababu, mfasiri anapofasiri hutakiwa kuweka mkazo kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.
Katika aina hii ya tafsiri, masahihisho au urekebishaji wa neno au jambo lolote unalodhani limekosewa haliruhusiwi isipokuwa unaweza kuweka hayo marekebisho au ufafanuzi katika tanbihi. Sasa tuangalie baadhi ya mifano ya aina hii ya tafsiri:
Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali
Kingereza: He went up to hospital
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: Jane alimwoa John
Aina hii ya tafsiri, ina faida kubwa katika ukuaji wa lugha lengwa kwa kuingiza miundo ya misemo kutoka lugha chanzi, mathalani, lugha ya Kiswahili imepokea miundo mipya ya misemo kutoka lugha ya Kingereza, baadhi ya miundo hiyo ni kama vile:
Kiswahili: Usiku mwema ? kutoka Kingereza: Good night
Kiswhili: Mabibi na mabwana ? kutoka Kingereza: ladies and gentlemen
Kiswahili: Wako mtiifu ? Kutoka Kiingereza: Yours Sincerel
Kiswahili: Naomba nichukue nafasi hii.. ? Kutoka Kiingereza: May I take this opportunity…
[Tazama pia Mwansoko na wenzake: 2006]
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano/ huru [Communicative Translation]
Hii ni aina ya tafsiri inayomlenga msomaji [hadhira] wa matini lengwa, ambaye katika aina hii ya tafsiri hatarajii kukutana na ugumu wowote katika matini atakayoisoma, bali hutarajia kukutana na tafsiri nyepesi ya dhana za kigeni katika utamaduni na lugha yake kwa kadiri itakavyoonekana. Hivyo basi, mfasiri wa aina hii ya tafsiri yuko huru kutafuta maneno na mafungu ya maneno yanayolingana na maneno, methali, nahau, utamaduni na mazingira ya lugha lengwa, pamoja na kuwa tafsiri ya kimawasiliano kufuata sarufi ya lugha lengwa ni lazima pia ifuate utamaduni, mazingira na historia ya jamii ya lugha lengwa. Tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: John alimwoa Jane
Kingereza: No need to cry over spilt milk
Kiswahili: Maji yakimwagika hayazoleki
Kiingereza: What comes around goes arround
Kiswahili: Mla vya watu, naye vyake huliwa.
Kiswahili: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
Kiingereza: A friend in need is a friend in need
Kiswahili: Bahati haiji mara mbili
Kiingereza: Golden chance never comes twice
Aina hii ya tafsiri hulenga kutoa athari ile ile au inayokaribiana kwa hadhira ya matini lengwa kama ilivyo kwa hadhira ya matini chanzi[ matini asilia], hii ni aina ya tafsiri ambayo hutumika sana kufasiri mawazo ya kigeni katika lugha na mazingira mapya, mawazo ambayo huelezwa katika misingi ya lugha, utamaduni na mazingira yanayoeleweka kwa hadhira ya matini lengwa.
Ebu tuangalie baadhi ya mifano tuliyoiangalia katika tafsiri ya Kisemantiki [maana] tunavyoweza kutafsiri katika njia ya tafsiri ya kimawasiliano:
Kiingereza Kiswahili
Good night Lala salama
Ladies and Gentlemen Ndugu zangu
Yours Sincerely Ni mimi
May I take this opportunity to… Naomba mnisikilize
Hivyo basi, katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hutafuta methali au misemo inayopatikana katika lugha lengwa inayohusiana au kukaribiana na ile ya lugha chanzi. Ebu jaribu kutafsiri misemo/methali zifuatayo ya lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza:
Adhabu ya kaburi aijuaye maiti
Asiyekubali kushindwa si mshindani
Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa
Chema chajiuza kibaya chajitembeza
Dua la kuku halimpati mwewe
Bandubandu humaliza gogo
Jogoo wa shamba hawiki mjini
La kuvunda halina ubani
Mtegemea cha nduguye hufa masikini
Faida ya aina hii ya tafsiri, humfanya mfasiri kuwa huru kutumia maneno au mafungu ya maneno ambayo huweza kutoa athari ile ile au inayokaribiana na maneno au mafungu ya maneno katika matini ya lugha chanzi, lakini mapungufu ya aina hii ya tafsiri huweza kutokea iwapo mfasiri ataamua kuegemea mno kwenye mawazo, historia, mazingira au itikadi ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: The Merchant of Venice
Kiswahili: Mabepari wa Venisi
Ukiangalia mfano huo utaona kuwa, The Merchant of Venice, tamthiliya iliyoandikwa na William Shakespeare, ingefaa pia kufasiriwa kuwa, Wafanyabiashara wa Venisi, lakini Mwalimu J.K Nyerere aliamua kuifasiri kuwa, Mabepari wa Venisi kutokana na kuwa Nyerere ndiye mwasisi wa itikadi ya Ujamaa nchini Tanzania, hivyo aliegemea katika itikadi kufasiri.
Hivyo basi, mtu anapokuwa anafanya kazi ya kufasiri, maandishi yo yote kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine atajikuta akiangukia katika moja wapo ya njia tulizozijadili hapo juu, lakini ikumbukwe tafsiri ya neno kwa neno ni nadra sana kutumiwa na wafasiri wengi, na njia hizo huweza kuingiliana katika matini moja ya tafsiri.
TATHMINI KATIKA TAFSIRI (TRASLATION CRITICISM)
Katika tafsiri tunafanya tathmini ili kujua ubora na upungufu wa tafsiri husika. Kutathmini tafsiri ni zoezi la kupima kiwango cha ubora wa tafsiri husika kwa kutumia mbinu zinazokubalika.
Tunapotathmini tafsiri tunaweza kupata makundi yafuatayo ya tafsiri hizo tunazotathmini;
· Tafsiri bora (good translation)
·Tafsiritenge/mbaya (mistranslation)
· Tafsiri finyu (under translation)
· Tafsiri pana (over translation)
TAFSIRI BORA; hii ni ile tafsiri ambayo kifani na kimaudhui inaendana na matini chanzi.
TAFSIRI TENGE; hii ni ile tafsiri ambayo haiendani na matini chanzi.
TAFSIRI FINYU; hii ni ile tafsiri ambayo imeacha vitu vingi katika kutafsiri.
TAFSIRI PANA; hii ni ile tafsiri ambayo imeongezwa mambo mengi ambayo hayapo katika matini chanzi au imefasiriwa kijumla jumla.
AINA ZA MATINI LENGWA ZINAZOFAA KUTATHMINIWA
Kuna aina mbili za matini lengwa ambazo zinafaa kutathminiwa kama ifuatavyo:
a) Matini lengwa zilizo katika mchakato wa kufasiriwa, hii ni ile matini ambayo bado haijafikishwa kwa walengwa. Mfasiri anaweza kutathmini upya matini kabla ya kuifikisha kwa mlengwa.
b) Matini zilizo mikononi mwa mtumiaji/mteja/hadhira. Fursa ya kuboresha kazi hiyo haipo ila hufanyiwa tathmini ili kutoa maoni ambayo yatamwezesha mfasiri kuboresha kazi nyingine zinazofuata au toleo linalofuata.
MBINU ZA KUTATHMINI TAFSIRI
1. Ulinganishaji wa matini; hii ndiyo mbinu kongwe zaidi na ndiyo inayotumiwa na wahakiki wengi zaidi (MC na ML). Katika mbinu hii kinachofanyika ni kwamba matini lengwa hulinganishwa na matini chanzi ili kubaini vipengele vya kimuundo na kimtindo vilivyoongezwa, vilivyopunguzwa au vilivyopotoshwa ili kuvifanyia marekebisho.
2. Kupima uasili; tafsiri bora haipaswi kusomeka kama tafsiri.
Hii ina maana kwamba mtu anaposoma tafsiri yako asijue kama ni kazi iliyotafsiriwa badala yake inatakiwa isomeke kama vile imeandikwa katika lugha lengwa hiyohiyo.
Hali ambapo tafsiri husomeka kama vile imeandikwa katika lugha lengwa hiyohiyo ndio ambayo huitwa uasili.
Hapa mfasiri mwenyewe au mtu mwingi anaisoma kazi hiyo. Inashauriwa apewe mtu mwingine tena bila kuambiwa kwamba kazi hiyo ni tafsiri.
3. Kupima uelewekaji; Katika mbinu hii kinachoangaliwa ni kueleweka kwa maudhui yanayotolewa katika tafsiri hiyo. Mtu anayepima uelewekaji atajiuliza yeye mwenyewe, je maudhui katika kazi hii yataeleweka kwa wasomaji au kazi hii inazungumzia nini? Hivyo inashauriwa kwamba mfasiri ampe mtu mwingine ili kuepuka kujipendelea. Tahadhari: Mtu anayepelekewa kazi hiyo inashauriwa awe mfasiri.
4. Kupima usomekaji; Katika mbinu hii ya kupima usomekaji mfasiri au mhakiki atapima tafsiri husika ili kuona iwapo inasikika vizuri masikioni mwa msikilizaji na kama inamtiririko unaokubalika katika lugha lengwa.
Hapa kunakuwa na watu wawili mmoja anasikiliza na mwingine anasoma kwa sauti.
5. Kupima ulinganifu; Katika hii mhakiki anaangalia umakini wa mfasiri katika kutumia kwa namna inayofaa vipengele muhimu vya matini kama vile msamiati, istilahi, maudhui au maneno muhimu yanayobeba maudhui.
Maana yake ni kwamba kama neno limejirudia rudia katika tafsiri usibadilishe, mfano: Aim – nia, lengo, madhumuni, kusudi, azma, shabaha, kusudi nk. Hivyo kama neno “Aim” umelifasiri kama lengo basi popote litakapojitokeza kwa mara nyingine katika matini basi libaki hivyohivyo bila kubadili badili.
6. Tafsiri rejeshi (Back Translation); Ni mchakato wa kutafsiri matini ambayo tayari imetafsiriwa katika lugha fulani yaani lugha lengwa na kuirejesha tena katika lugha chanzi kwa lengo la kuitathmini tafsiri hiyo.
UKALIMANI
Ukalimani ni nini?
Ukalimani ni uhawalishaji wa taarifa au ujumbe kutoka kwa msemaji wa lugha chanzi kwenda katika lugha lengwa kawa njia ya mdomo au mazingumzo.
Katika ukalimani matini chanzi huwa katika mazungumzo na matini lengwa pia huwa katika mazungumzo.
Katika ukalimani mkalimani hana muda wa kutosha wa kujiandaa kwa sababu anatakiwa kukalimani kile anachosikia wakati ambapo mzungumzaji anaendelea kuzungumza mambo mengine.
Aina za ukalimani
Kuna aina mbalimbali za ukalimani kutegemeana na vigezo unavyotumia kuainisha au kupata hizo aina;
1. Kigezo cha kwanza ni kigezo cha Muktadha;
Katika kigezo hiki vipengele vinavyojitokeza ndani ya muktadha ili kupata aina tunazingatia mahali, lengo, aina ya hadhi, sifa za walengwa nk.
1.Ukalimani wa Kijamii/community interpretation: Huu ni ukalimani ambao hufanywa katika masuala mbalimbali ya kijamii kama vile afya, ujenzi wa shule huduma za kijamii kama vile maji, umeme, masuala ya mihadhara ya kidini nk.
2.Ukalimani wa Mikutano au Makongamano/Conference; Huu ni ukalimani unaofanyika katika makongamano au mikutano mbalimbali. Mara nyingi aina hii ya ukalimani inafanyika katika mikutano ya kimataifa.
3.UkalimaniwaMahakam.
Aina hii hufanywa na wanasheria katika mahakama za ngazi mbalimbali. Pia huitwa ukalimani wa kisheria.
4.Ukalimani wa Kitabibu; Huu ni ukalimani ambao unafanyika mahali ambapo matibabu yanapatikana, kwa kiasi kikubwa aina hii ya ukalimani inafanyika katika hospitali kubwa kubwa.
5.Ukalimani wa Habari/katika vyombo vya habari; Huu ni ukalimani unaofanywa katika vyombo mbalimbali vya habari, hususani redio na televisheni ili kuiwezesha hadhira lengwa iweze nayo kuelewa matangazo yanayotolewa kwa lugha chanzi.
6.Ukalimani Sindikizi/Escort interpretation; Katika aina hii ya ukalimani mkalimani hufuatana na mtu au kikundi cha watu katika safari au katika usaili au mahojiano.
2. Kigezo cha pili ni kigezo cha Muundo au Mfumo wa Lugha/Language mode/modality;
Katika kigezo hiki lugha inayotumika katika ukalimani inaweza ikawa lugha ya kusema/kizungumza na lugha ya alama.
Kupitia lugha ya alama tunapata aina moja ya ukalimani yaani ukalimani wa viziwi
Kwa kupitia lugha ya mazungumzo au kusema tunapata aina mbili za ukalimani ambazo ni;
1.UkalimaniMfululizo/Andamizi/Simultaneous interpretation; Katika ukalimani mfululizo, kama jina lenyewe linavyodokeza mkalimani huzungumza takribani sambamba na mzungumzaji wa lugha chanzi. Katika aina hii ya ukalimani mkalimani lazima afanyekazi kwa haraka sana ili kuendana na kasi ya mzungumzaji kuepuka kupitwa na mambo muhimu.
Katika ukalimani mfululizo makalimani huketi katika chumba maalum cha ukalimani (booth) ambacho hakipitishi sauti (sound proof) na kisha huzungumza kwa kutumia kipaza sauti huku akimwona na kumsikia mzungumzaji wa lugha chanzi kupitia visikizio (ear phone.
2.Ukalimani Fuatishi/Mtawalia (Consecutive interpretation); Katika ukalimani fuatishi makalimani huzungumza/hukalimani baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kumaliza ujumbe wake au hata kama hajamaliza ujumbe wake baada ya mzungumzaji wa lugha chanzi kutulia kwa sekunde kadhaa ili kumpa makalimani fursa ya kukalimani kile kilichosemwa. Katika aina hii mkalimani na mzungumzaji wa lugha chanzi mara nyingi wanakuwa pamoja wakiwa wamesimama kwenye jukwaa au wakiwa wameketi mezani.
SIFA ZA MKALIMANI BORA.
· Awe na ujuzi wa hali ya juu wa lugha anazoshughulika nazo pamoja na utamaduni wake.
· Ajue lugha zaidi ya mbili za kimataifa kwani kadiri unavyojua lugha zaidi ndivyo unavyokuwa mkalimani bora zaidi.
· Awe na ujuzi au maarifa ya kutosha juu ya mada, taaluma au uwanja unaozungumziwa.
Inamaana kwamba kama wewe ni mfasiri wa masuala ya kiuchumi basi hupaswi kufasili masuala ya kisheria. Mfano; ukalimani wa mahakamani hufanywa na wanasheria.
· Awe na ujuzi wa taaluma ya ukalimani; yaani awe amepata mafunzo ya ukalimani. Katika hayo mafunzo atajifunza mbinu za ukalimani aina, changamoto na namna ya kuzikabili.
· Mfasiri anatakiwa awe mchapakazi, mdadisi na apende kujiendeleza au kupata habari kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii mfano; magazeti, majarida, televisheni, facebook, twitter au kuzungumza na watu/kuchangamana na watu.
· Awe na kipaji, yaani:
Uwezo wa kukumbuka
Kuteua msamiati sahihi kwa haraka
Kipaji katika kuunda istilahi haraka haraka na kuitumia.
Kipaji cha ulumbi/awe na ulumbi yaani kipaji cha kuongea na kuvuta watu (eloquency)
· Awe na uzoefu.
UMUHIMU WA UKALIMANI
1. Ukalimani ni daraja linalosaidia kuunganisha watu au jamii inayozungumza lugha tofauti.
2. Ukalimani ni nyenzo ya kueneza utamaduni. mfano; dini
3. Ukalimani husaidia katika masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa. Mfano; usuluhishi wa migogoro.
4. Ukalimani hutumiwa na makampuni ya simu kuwasiliana na wateja wao
5. Ukalimani husaidia kufanikisha vikao, mikutano na makongamano ya kitaifa na kimataifa. Mfano; mikutano ya UN, AU nk.
6. Ukalimani hutumika kama mbinu ya kijifunzia lugha ya pili au lugha ya kigeni hasa katika hatua za awali.
7. Ukalimani unamsaidia mkalimani mwenyewe kujifunza lugha.
STADI MUHIMU KATIKA UKALIMANI
i) Lugha na mawasiliano;- kumudu stadi za lugha na mawasiliano
ii) Kuwa na stadi ya kusikiliza
iii) Stadi ya kudondoa (kuandika muhtasari) – kuchukua mambo muhimu tu kati ya mengi anayoongea.
iv) Stadi ya kumbukumbu/kukumbuka (memory rehesion skill)
v) Sanaa ya kuzungumza hadharani. mfano; jinsi ya kuandaa hotuba, jinsi ya kuanza kwa kishindo, jinsi ya kumaliza kwa kishindo, kutoa mifano dhahiri, kuepuka kujisifia, Toa visa vya kweli/mara nyingi inashauriwa kutoa visa vyako/vinavyokuhusu wewe, kuepuka vitabia vinavyokera mfano; kuchokonoa puani, kujikuna kuna nk.
vi) Hakikisha umevaa vizuri nk.
TAFSIRI NA UKALIMANI:
KUFANANA NA KUTOFAUTIANA
Tofauti kati ya tafsiri na ukalimani: vipengele/vigezo vya kutofautisha dhana hizi mbili;
a) Dhana (maana/fasili)
b) Lugha (mtindo, stadi maalum nk)
c) Utendaji (mf; vifaa/zana)
d) Kigezo cha mada/maandalizi/uhawilishaji
e) Mfumo wa lugha (kuzungumza au kuandika)
f) Uwasilishaji (mara moja tu au kuna nafasi ya kudurusu)
g) Hadhira (papo kwa papo au mbali)
h) Maslahi/malipo (utaratibu wa kutoza pamoja na tozo lenyewe/bei mf; kwa ukurasa au maandishi/saa.
i) Ukongwe/umri/historia (kipi kilianza)
j) Stadi muhimu za lugha zinazohitajika. mfano; kusoma, kuandika, kusikiliza na kuzungumza.
KUFANANA KWA TAFSIRI NA UKALIMANI
a) Vigezo
b) Njia (kibebeo)
c) Lengo/dhima
d) Vijenzi (vipengele vya modeli/muundo wa mawasiliano, mfano; sender – channel – receiver – feedback.
e) Faida
MAREJEO:
Cartford, J. C. (1965). A Linguistic Theory of Translation. London: OUP.
Larson, L. M. (1984). Meaning-based Translation. London: University Press of America.
Mwansoko, H. J. M. na wenzake (2006). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu Dar es Salaam: TUKI.
Newmark, P. (1982). Approaches to Translation. Oxford: Pergamon Press.
Newmark, P. (1988). A Textbook of Translation. London: Prentice Hall.
Nida, E. A. (1964). Towards a Science of Translation. Leiden: E. J. Brill.