KISWAHILI KIDATO CHA TATU: KUKUA NA KUENEA KWA KISWAHILI NCHINI TANZANIA ENZI ZA WAARABU NA WAJERUMANI


KUENEA KWA KISWAHILI NCHINI TANZANIA WAKATI WA WAARABU NA WAJERUMANI NHINI TANZANIA

Wageni walipokuja pwani ya Afrika mashariki waliwakuta wenyeji tayari wana lugha yao ya mawasiliano ambayo ni Kiswahili na pia lugha hiyo ilikuwa inatumika katika shughuli za kibiashara miongoni mwao.

 Kwahiyo wageni walipofika pwani ya Afrika mashariki hawakuona sababu ya kutumia lugha nyingine zaidi ya Kiswahili katika shughuli zao mbalimbali.

pia wageni waliofika pwani ya Afrika mashariki, walifika kwa nyakati tofauti tofauti na walifika wageni kama vile waarabu, wareno, wajerumani na waingereza na wageni hawa kuna baadhi walikiendeleza Kiswahili na wengine walikidumaza Kiswahili

KUKUA NA KUENEA KWA KISWAHILI ENZI ZA WAARABU



Swali:   Eleza mambo mbalimbali yaliyo changia ukuaji na ueneaji wa kiswahili nchini Tanzania wakati wa utawala wa waarabu.


Kuenea kwa lugha ni kuongozeka kwa watumiaji. Wageni wa kwanza kuja pwani ya Afrika mashariki ni waarabu na kutokana na kuingiliana na wabantu katika Nyanja mbalimbali Kiswahili kilichukuliana maneno na kuathiriana na lugha ya kiarabu

Sababu zilizochangia kukua kwa Kiswahili enzi za waarabu

·         Biashara – Waarabu walipowasili katika mwambao wa pwani ya Afrika mashariki walianza kufanya biashara na wabantu. Kutokana na maingiliano hayo Kiswahili kilianza kupanuka na kuongozeka misamiati kwa hiyo bila shaka Kiswahili kilikuwa kutokana na maingiliano hayo. Mfano wa msamiati uliochukuliwa katoka kwa waarabu ni kama vile jahazi, kodi, adesii n.k

·  Utawala – waarabu pia walitumia Kiswahili katika shughuli mbalimbali za kiutawala. 

 Waarabu walitawala Zanzibar, sehemu za pwani ya bara na pemba kutokana na shughuli za kiutawala kuna maneno ya kiarabu ambayo yameingia kwenye Kiswahili. Mfano; mwinyi, sultani, mtukufu, enzi n.k


·         Dini – Hali kadhalika walipowasili walianzisha dini yao ya kiislamu kwenye upwa wa Afrika kwa kutumia lugha ya Kiswahili. Waafrika walifundishwa kuandika na kusoma kwa hati za kiarabu ili waweze kusoma na kuelewa kurani. 

Hivyo wakajikuta wanaingiza baadhi ya maneno ya kiarabu kwenye lugha ya Kiswahili. Baadhi ya maneno ni kama vile elimu, alasiri, alfajiri n.k

·  Ndoa – wageni hawa pia walipofika pwani ya Afrika mashariki waliishi kwa miaka mingi na hivyo kuchangamana na wenyeji na baadae waarabu wakaoa wanawake wa kibantu na hata vizazi vyao vilipozaliwa. 

 Walitumia lugha ya Kiswahili katika mawasiliano yao na pia hata utamaduni wao ulijiegemeza kwenye lugha ya Kiswahili. Hata jamii ya watu wa pwani waliwaita watoto wao waswahili badala ya maneno kama vile chotara, kwahiyo kutokana na hivyo basi ndoa kati ya waarabu na wabantu ulichangia kwa kiasi kikubwa kukua na kuenea kwa waswahili

KUKUA NA KUENEA KWA KISWAHILI ENZI ZA UTAWALA WA WAJERUMANI NCHINI TANZANIA


Swali: Eleza shughuli za wajerumani zilizo saidia kukua na kueneza kiswahili nchini Tanzania

Wajerumani pia walitawala Tanganyika kwa muda wa miaka 30 na walipofika walikuta Kiswahili kimekua sana katika nchi za Afrika mashariki kwahiyo walipofika Tanganyika walitumia lugha ya Kiswahili kama chombo cha mawasiliano katika shughuli zao mbalimbali za utawala na hata kwenye kutolea elimu kwa ajili ya manufaa yao.

Pia mfanyakazi yeyote wa kiafrika ili kupata kazi ilimbidi ajue Kiswahili kwa kuongea na kuandika ndipo apate kazi pia ripoti zote za utawala wa kijerumani zilitakiwa kuandikwa kwa Kiswahili.

Vilevile wanafunzi waliohitimu walisambazwa sehemu mbalimbali nchini na kwa njia hiyo kiswahili kilikua na kuenea sana halikadhalika mashamba yaliyoanzishwa na wajerumani yalikuwa na wafanyakazi mchanganyiko kutoka sehemu mbalimbali na lugha ya mawasiliano miongoni mwao ilikuwa ni kiswahili kwa hiyo walichukua na baadhi ya msamiati kutoka kwenye kabila zao na kuingiza kwenye Kiswahili na hivyo kuchangia ukuaji wa Kiswahili

MBINU ZILIZOTUMIKA KUENEZA KWA KISWAHILI NCHINI TANZANIA WAKATI WA UTAWALA WA WAJERUMANI

Mahakama – utawala wa kijerumani ulitumia pia lugha ya Kiswahili katika shughuli zake kwa hivyo kazi zote ziliendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na pia wafanyakazi na wazee na mahakani walihoji na kutoa hukumu kwa watuhumiwa kwa kutumia lugha ya Kiswahili na hivyo kuchangia kukua na kuenea kwa lugha ya Kiswahili

Elimu – mashuleni pia Kiswahili kilitumika kama lugha ya kufundishia na kijerumani kilifundishwa kama somo la kawaida tu katika shule za msingi.

Wajerumani walijenga shule sehemu za tabora, ujiji, kilimatinda, mpwapwa, kasangu mwaka 1905, iringa, mwanza, bukoba, kilosa, tukuyu, na moshi pia vyuo vya kufundishia walimu vilianzishwa huko tabora na bukoba hivyo basi walimu na wanafunzi walijifunza na kukitumia Kiswahili katika shughuli zao za elimu na kusababisha kuenea na kukua kwa Kiswahili

Utawala – wajerumani walipofika nchini walikuta lugha ya Kiswahili imekua na kuenea sana hivyo nao katika utawala na hivyo kuamua kujifunza Kiswahili kabla ya kuja nchini na pia hapa nchini wajerumani walitoa mwongozo kwa viongozi wa nchini kwa kutumia lugha ya Kiswahili na hivyo viongozi wote wa kiafrika mfano akida, jumbe n.k walitakiwa kujifunza lugha ya Kiswahili kwasababu walikuwa wanatumwa sehemu mbalimbali sio nchi walikozaliwa tu hivyo kuchangia kukua na kuenea kwa haraka.

Shughuli za kilimo (mashamba) – wajerumani pia walianzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara na kuwalazimisha watu wafanye kazi kwenye mashamba hayo mfano, mashamba ya katani Tanga, kahama, Kilimanjaro kwahiyo kwenye mashamba hayo kulikuwa na idadi kubwa ya watu kutoka sehemu mbalimbali na lugha yao ilikuwa ni Kiswahili kwahiyo wale waliobahatika kurejea majumbani mwao walisaidia kukieneza Kiswahili kwasababu waliendelea kutumia lugha ya kiswahili.