KISWAHILI KIDATO CHA PILI MADA YA PILI: MATUMIZI YA LUGHA KATIKA MIKTADHA MBALIMBALI MATUMIZI YA LUGHA

MATUMIZI YA LUGHA
 Hii ni namna au jinsi ya matumizi ya lugha, mila, desturi na taratibu za jamii. Ni jinsi ambavyo mzungumzaji anaweza kutumia lugha yake kuhusiana na msikilizaji.

Hivyo basi, lugha hutegemea mambo yafuatayo: -
Uhusiano wa mzungumzaji na msikilizaji (wazungumzaji)
Mada inayozungumziwa
Mazingira
Dhumuni la mazungumzo husika.

UMUHIMU WA MATUMIZI YA LUGHA
Lugha humsaidia msomaji wa kawaida au mwanafunzi kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.
Lugha humsaidia msomaji wa kawaida au mwanafunzi kutofautisha na kutumia mitindo mbalimbali katika lugha ya Kiswahili

MATUMIZI YA LUGHA HUTAWALIWA NA MAMBO YAFUATAYO: -
MAZINGIRA
Msomaji anayetumia lugha yeyote ile kwa kawaida huwa katika mazingira yanayomtawala kimaisha, mazingira ya namna hiyo ndiyo yanayomuamulia kuhusu vitendo atakavyotumia na hata mazungumzo yake.
 Kutokana na mazingira tunapata: -
Lugha ya shuleni
Lugha ya hotelini
Lugha ya sokoni
Lugha ya ofisini
Lugha ya mtaani
Lugha ya msikitini
Lugha ya kanisani.
UHUSIANO BAINA YA WAHUSIKA
Uhusiano kati ya wahusika wanaotumia lugha nao unaathiri uzungumzaji wa lugha, mazungumzo au lugha itakayotumika hutegemea wanavyoongea.
Kutokana na uhusiano wa wahusika tunapata tunapata yafuatayo: -
Lugha kati ya mtoto na mama au baba
Lugha ya watu wa rika linalolingana
Lugha ya mwalimu na mwanafunzi.
Lugha kati ya wapenzi.
Kwa kawaida baba ataongea lugha ya kuamuru dhidi ya mtoto na mtoto atajibu kwa unyenyekevu na ndivyo ilivyo pia kwa mwalimu na mwanafunzi wake au bosi na mfanyakazi wake.
Kwa mfano: -
Lugha ya watu wa rika linalolingana huzungumza lugha ambayo wanaelewana wenyewe na siyo rahisi mtu wa rika tofauti kuelewa lugha hiyo.
Kwa mfano: -
” Mshkaji tunasikia hutingi skonga siku hizi”
” Dah si Yule ticha mnoko ananiletea mapichapicha.... eti kanipakazia ni mchapa daftari wa shule, noma kweli mwana” Maticha wetu wanapanga wanipe kibano lakini nikachora mbio”
” Chekini wachizi, mshua angeniona si ingekuwa msala!'
MADA YA MAZUNGUMZO
Mada ya mazungumzo fulani hutawala jinsi ya mazungumzo na uzungumzaji kwa ujumla. Kutokana na mada husika katika mazungumzo tunapata lugha ya: -
Kitabibu
Biashara
Kisiasa
Mahubiri
Kitaaluma
Kisheria
Kwa mfano:
Musa: John, ili kufaulu somo langu la Kiswahili inanipasa nifanye nini?
John: Lazima usome kwa bidi na maarifa.

MADHUMUNI YA MAZUNGUMZO
Hapa anayezungumza hutoa ufafanuzi wa jambo anayotaka kusema.
Hivyo, ufafanuzi wa jambo husika utategemea;
Mazingira
Mada ya mazungumzo
Uhusiano baina ya mzungumzaji na msikilizaji
Kwa mfano:
Mhadhara au mazungumzo ya kiuchumi ya Tanzania yanatofautiana kabisa na mhadhara au mahubiri msikitini au kanisani.
JINSI YA MAZUNGUMZO
Namna mawasiliano yanayowasilishwa kwa njia ya maandishi au mazungumzo ya mdomo kwa kwaida huathiri jinsi au mtindo wa uzungumzaji.
Kwa mfano: -
Kwa mfanyabiashara kwa vyovyote atapamba uzungumzaji wake ili kuwavutia wateja wengi.
"Mpendezeshe mwanao kwa mia tano, na mpendezeshe mkeo kwa elfu moja"
REJESTA
Rejesta ni mtindo wa lugha unaotumika mahali fulani penye shughuli ambayo ni tofauti na lugha ya kawaida
AINA ZA REJESTA
(i) Rejesta za Mitaani/kijiweni
Haya ni mazungumzo yanayozungumzwa magengeni nayo hueleweka na wazungumzaji wenyewe. Ni lugha ambayo huchipuka kutokana na kikundi cha watu ambacho ni kidogo.
Lugha hii hudumu kwa muda mfupi tu, halafu hufifia. Wakati mwingine lugha hiyo hukubaliwa na jamii na kuweza kuingizwa katika msamiati wa lugha hiyo.
Mfano wa maneno yanayotumika sana mitaani ni kama vile:-
 “Mshikaji” (rafiki) Demu” (mwanamke), “Nina waya” (sina pesa), “Kumwaga unga” (kupoteza kazi), umenoa” (umekosa), (mambo safi), n.k. Kwa ujumla lugha  ya mitaani ni lugha isiyo sanifu, ni lugha iliyojaa maneno ya mitaani ambayo yanaeleweka wa wazungumzaji wenyewe.
Mfano:
Ee bwana we! Maana hiyo Benzi ilikuja kitututu-wangu wangu! Bila kutazama mbele kunakuja nini, basi akamwingia babu wa watu-akamrusha kama mpira,  alipofika chini, kwisha habari yake! Kichwa kama chapati. Simbaa wa mji watatumaliza...
 (ii) Mazungumzo ya Kwenye Shughuli Maalum (Rejesta za Mahali)
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu hayafanywi kiholela, bali yanafuata taratibu na kanuni maalum zinazojitokeza katika mazingira haya. Kutokana na kutumiwa kwake kwa muda mrefu kwenye mazingira yale yale.
Mazungumzo ya kwenye shughuli maalumu ni kama vile mazungumzo ya:
 Maofisini au mahali popote pa kazi
  Mahakamani
  Hotelini
 Hospitalini
  Msikitini
Kanisani  n.k
 (a)      Mazungumzo ya mahotelini yana utaratibu wake ambao katika hali ya kawaida inaweza isieleweke.
Mfano:
A:     Nani wali kuku
B:    Mimi
A:    Chai moja wapi?
B:    Hapa
Katika mazungumzo haya A anapouliza “Nani wali kuku”: ana maana kuwa nani anahitaji kula wali na nyama ya kuku”. Hapa hana maana ya kumwainisha mtu aitwaaye “wali kuku”.
 (b)   Kwa upande wa lugha ya mahakamani ni tofauti a lugha ya hotelini. Lugha ya mahakamani inasisitiza  usahihi ili kuondoa migongano miongoni mwa wanaohusika.
Mfano:
Wakili wa Utetezi: Nakuuliza jaribio la kutaka kupindua serikali litakuwa kosa la namna gani katika sheria za Kenya?
Kamishna Msaidizi: (Baada ya kupewa kitabu cha sheria za Kenya na kukisoma) Ni kosa la uhaini.
Wakili wa Utetezi:  Ulichukua muda mrefu kufikia jibu hili. Washitakiwa wawili hawahusiani na makosa haya?
Kamishna Msaidizi:    Sijui. (Uhuru, 26 Agosti, 1982:4).
Kimsingi hii ni hali ya kawaida kabisa katika mahojiano ya mahakamani. Mara nyingi mahojiano katika mahakama hayaendi haraka sana. Kila mtu anayehusika – hakimu, mwendesha mashtaka, wakili, mdaiwa, shahidi, n.k. hujieleza kwa wazi wazi bila kujali urefu wa maelezo.
 (iii) Rejesta Zinazohusu Watu
Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi ni yale maongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi; kwa mfano mazungumzo kati ya:
-         Vijana wenye rika moja,
-         Wazee wenyewe,
-         Wanawake wenyewe,
-         Wanaume wenyewe,
-         Mwalimu na mwanafunzi,
-         Meneja na wafanyakazi wake,
-         Mtu na mpenzi wake, n.k.
(c)        Mazungumzo miongoni mwa marafiki wa rika moja huzungumza lugha ambayo wao wenyewe wanaielewa na sio rahisi kwa mtu wa rika lingine kuielewa lugha hiyo.
Mfano:
‘Basi,  Master jana wikiendi ilikuwa kibaridi sana’
‘Basi nilizamia infoo kwenye zinga la mnuso huko saiti za upanga’
‘Nilifika getini nikakuta baunsa kanyuti chedro likisubiri kumtoa
noma kila mzamiaji’
Alikuwa mnoko kishenzi’
‘Akatema mkwala mbuzi, nikajibu kwa mkwala  dume....
akabloo mimi ndani’.
Maana ya Maneno
Wikiendi – Mwisho wa wiki.
Kibaridi –tulivu.
Kuzamia infoo – Kuingia mahali bila kualikwa.
Zinga la Mnuso –sherehe kubwa.
Saiti –sehemu.
Baunsa limenyuti chedro – Ni mlinzi wa mlangoni ametulia pembeni.
Noma – Hatari.
Mnoko kishenzi – kinaa sana
Mkwala mbuzi – Vitisho dhaifu (Sani, Toleo Na 49).
 Mtu asomapo maelezo hayo, mara moja unaona jinsi vijana hawa wa rika moja waishio mjini wanavyozungumza Kiswahili. Si rahisi kwa mzungumzaji wa Kiswahili sanifu kuielewa kirahisi lugha hiyo.
Mfano mwingine wa wazungumzaji wa Kiswahili wa rika moja. Mzungumzaji Mkuu ni Chek Bob.
Yee! Mjumbe, degree kama degree mimi oyee tu. Nadhania umeiget fresh kuhusu nguvu-nguvu kazi au vipi?. Mimi ndo longtime niko hapa town bila Job nadunda na mensheni tu. Na vile vile ndo nina wiki ee tu tangu niopoe hiki kikwapa. Wewe mwenyewe ukikicheki kikwapa chenyewe waa! Sasa kwende nacho bush nishai au vipi mjumbe? Serikali yeneywe inatutia mikwala sana. Sasa shika hivi visimbi vya anda bee na kitembo (210) kusudi mimi nibane hapa hapa town. Hawa kinaa watilie mikwala mingi kwamba mimi ndo longtime nina Job. Kwani misheni hii ikijipa utaipata wewe mwenyewe mjumbe!. (Mfanyakazi Machi, 1988). Huu ni mfano mwingine wa kijana wa mjini, lakini anamweleza mjumbe hisia na maoni yake.
  (iv) Lugha ya Kitarafa
Hiki ni Kiswahili cha tarafa fulani. Ukikisema katika tarafa nyingine huwa ni vigumu watu wa sehemu hiyo kuelewa unasema nini. Kwa ujumla ni Kiswahili ambacho kimeathiriwa na vilugha, yaani lugha-mama.
Kwa mfano:
Kiswahili cha Kiyao – John amenitona (amenifinya).
Kiswahili cha Kingoni – Mtambo mrefu (muda mrefu).
Kiswahili cha Kimakonde – Achante chana (asante sana).
Kiswahili cha Kinyakyusa – Kyama Kya Mapindusi (Chama cha Mapinduzi), n.k.
 (v) Kiswahili Rasmi/Sanifu
Ni msawazisho kutokana na vilugha vya lugha ya Kiswahili. Kiswahili hiki hukubaliwa na wengi katika nchi na ndicho kitumikacho katika shughuli za  kiserikali, kisiasa, elimu, uchumi, na vyombo vya habari hutumia lugha hii. Mtu akizungumza lugha rasmi ni vigumu kumtambua anatoka sehemu gani ya nchi. Kiswahili rasmi nchini Tanzania kinatokana na lahaja ya Kiunguja.
 DHIMA (MATUMIZI) YA REJESTA
  (i) Rejesta Hutumika Kama Kitambulisho
Rejesta hutofautisha mtindo wa lugha miongoni mwa wazungumzaji. Rejesta inawatambulisha wazungumzaji kuwa wao ni kundi fulani.
Mfano: Rejesta yawahunzi inawatambulisha kuwa wao ni tofauti na wavuvi ambao nao pia wana rejesta yao. Rejesta ya kanisani au msikitini ni tofauti na rejesta ya jeshini, n.k.
(ii) Rejesta Hupunguza Ukali wa Maneno
Rejesta inapotumiwa na kundi la watu, huficha jambo hilo linalozungumziwa lisieleweke kwa wengi. Hivyo hadhira inapuuzwa kwa sababu siyo watu wengi wanaoelewa.
(iii) Rejesta Inatumika Ili Kurahisisha Mawasiliano
Rejesta inatumika ili kurahisisha mawasiliano au kupunguza muda wa kuwashughulikia watu au wateja wengi. Kwa mfano mganga anayegawa dawa hospitalini anaposema “mbili asubuhi, mchana na jioni” akiwa na maana kuwa mgonjwa anywe vidonge viwili asubuhi, viwili mchana na viwili jioni. Hapa amefupisha ili aweze kuwahudumia kwa wakati mfupi wagonjwa wengi wanaosubiri kupata dawa.
(iv) Rejesta Hupamba Lugha Miongoni mwa Wazungumzaji
Kwa mfano,
Rejesta ya Hotelini.
Mhudumu: Nani wali kuku?
Mteja: Mimi hapa!
Mhudumu: Nani ugali-ng’ombe?
Mteja: Mimi hapa!
Mazungumzo haya kati ya mhudumu na mteja licha ya kurahisisha mawasiliano, vilevile yanapamba mazungumzo hayo.
(v) Rejesta Huweza Kuwa Kiungo cha Ukuzaji wa Lugha
Kutokana na matumizi ya rejesta mbalimbali, lugha inayohusika inaweza kuunda msamiati wake. Kuna baadhi ya maneno ya lugha yanayotokana na rejesta mbalimbali.
MAMBO YANAYOSABABISHA KUTOKEA KWA REJESTA
 (i) Ubinafsi
Ubinafsi ni tabia aliyonayo mtu, iwe ya muda au ya kudumu. Kila mtu ana namna ya kusema na kuandika au kuzungumza, ambayo humtofautisha na watu wengine. Hali hii huleta ubinafsi katika sauti yake (matamshi), msamiati, maandishi yake na mwisho huleta mtindo wa kipekee ambao ni tofauti na watua wengine. Hii ni sababu ya kwanza inayosababisha rejesta katika lugha. Hapa tunapata rejesta za watu.
(ii) Maingiliano
Makundi ya watu mbalimbali yanapochangamana husababisha mwingiliano miongoni mwao. Na ili kuweza kutofautisha kundi moja na kundi jingine kuna mambo fulani fulani ambayo hutofautiana miongoni mwa makundi hayo na mambo haya huweza kuwa ya kipekee katika kundi moja tu. Mambo hayo katika lugha huhusisha matamshi ya maneno, sarufi (mpangilio wa maneno) n.k. Tofauti hizi husababisha mitindo miwili tofauti miongoni mwa makundi hayo – hivyo husababisha kuzuka kwa rejesta.
(iii) Kupita kwa Wakati
Kila mahali katika jamii, hujitokeza mitindo katika kipindi maalumu. Na hii ni kutokana na mabadiliko ya kihistoria yanayoikumba jamii fulani. Kila kipindi cha mpito wa kihistoria huweza kuwa na maneno yake ambayo huwa ni tofauti na kipindi kingine cha kihistoria. Vilevile mitindo ya lugha kutoka kipindi kimoja hadi kipindi kingine huweza kuwa tofauti. Hivyo, rejesta huweza kutokea kati ya kipindi kimoja na kipindi kingine. Mfano, kipindi cha enzi za Ukoloni na kile cha Uhuru, kipindi cha enzi za Azimio la Arusha na kile cha Hali Ngumu ya Maisha au, na kile cha Mfumo wa Mageuzi.
(iv) Shughuli Iliyopo
Hapa hutegemea ni mazingira gani ambapo shughuli hiyo inafanyikia. Mfano misikitini, makanisani, dansini, bandarini, mahakamani, shuleni, nk. Shughuli fulani katika mazingira fulani hutupatia rejesta za mahali.
(v) Tofauti za Hadhi za Wahusika (Uhusiano wa Wahusika)
Mfano wasomi/wasiosoma, mwajiri/mwajiriwa, tajiri/maskini. Hii hali kwa ufupi husababishwa na matabaka yaliyopo katika jamii, tabaka moja na tabaka jingine hutumia lugha ambayo huwa ni tofauti miongoni mwao, na hivyo husababisha rejesta kuzuka miongoni mwa matabaka hayo.
 (vi) Matumizi ya Uficho/Tafsida
Hali hii pia husababisha kuzuka kwa rejesta kwani husababisha mitindo mbalimbali ya lugha miongoni mwa wazungumzaji. Kwa mfano vijana wanaweza kutumia maneno haya “silaha yake haina risasi, silaha yake ni butu, silaha yake haiwezi kukata hata kipande cha mkate” wakimaanisha kwamba “uume wake haufai”.
Au
Vijana wa mitaani huweza kusema “Yule anti ni mkarimu kweli kweli, ni mama huruma – anawahudumia vijana wengi, huwashibisha kwa kuwalisha chakula kinono kweli kweli”–wakimaanisha “binti ambaye akitongozwa humkubali kila mwanamme.”
ZINGATIA
i. Rejesta ni mtindo wa lugha inayotumika mahali penye shughuli fulani ambayo ni tofauti na lugha ya kawaida. Rejesta ya wavuvi, ya washairi, ya wafanyabiashara, ya wahuni, n.k. ni baadhi tu ya mifano. Rejesta zinazotokana na umri, kwa mfano, vijana wana rejesta yao, na wazee wana yao.
ii. Rejesta inayotokana na jinsia, kwa mfano, wanawake wana rejesta yao mbali na ile ya wanaume.
iii. Rejesta zinazohusu watu ni yale mawasiliano yasiyo rasmi ni yalemaongezi ya kawaida ya kila siku au mazungumzo rasmi;
kwa mfano mazungumzo kati ya:
- Vijana wenye rika moja,
- Wazee wenyewe,
- Wanawake wenyewe,
- Wanaume wenyewe,
- Mwalimu na Mwanafunzi,
- Meneja na Wafanyakazi wake,
- Mtu na Mpenzi wake, n.k.
- Marafiki nao wana rejesta yao.
- Rejesta ya mitaani au vijiweni. n.k.
MISIMU / SIMO
Misimu ni semi za muda na mahali maalum ambazo huzuka na kutoweka kutegemea mazingira maalum. misimu inayodumu huweza kuingia katika methali, nahau au misemo ya lugha ya jamii hiyo.
CHANZO CHA MISIMU
Misimu huzuka kutoka na na mabadiliko ya kihistoria yanayokumba jamii katika nyakati mbalimbali.
Misimu mingine huzuka kutokana na hali ya utani miongonim mwa watu mbalimbali.
Mara nyingi misimu ya aina hii hubeba kebehi, dhihaka, kejeli, mabezo, dharau au kusifu kusiko kwa kawaida.
SIFA ZA MISIMU
Misimu huzuka na kutoweka.
Misimu ni lugha isiyo rasmi.
Misimu ni lugha ya mafumbo.
Misimu ina chuku nyingi.
Misimu ina maana nyingi.
Misimu hupendwa sana na wengi.
Misimu ina mvuto na kwa sababu hii hupendwa na watu wengi.
Misimu huhifadhi historia ya ya jamii.
SABABU ZA KUTUMIA MISIMU
Kutaka mazungumzo yawe siri.
Kudhania matumizi ya misimu ndio ujuzi wa lugha.
Kufanya mambo mazito naya maana kuwa mepesi naya kawaida.
NJIA ZITUMIKAZO KUUNDA MISIMU
Njia ya kufupisha maneno (Kufupisha maneno mfano Kompyuta –komp)
Njia ya kutohoa kutoka lugha za kigeni. (Kutotoa maneno ya kigeni mfano father- fadhee)
Njia ya kutumia sitiari (Kutumia sitiari au jazanda mfano-Golikipa –Nyani, Mtu mlafi-fisi)
Njia ya kutumia tanakali (Kutumia tanakalimfano; Bunduki – mtutu)
Njia ya kubadili maana ya msingi
AINA ZA MISIMU
Misimu ya pekee
Huelezea uhusiano uliopo kati ya kikundi kimoja kutoka kwenye utamaduni mmoja. Misimu hii inapatikana sehemu fulani ambapo wanaishi watu wa aina moja, mfano kazini. Misimu hii inaitwa ya kipekee kwa sababu hujulikana sehemu ilipozukia tu, na sio nje ya eneo hilo.
Kwa mfano misimu ya kipekee inaweza kutumiwa na: -
Wafanyakazi katika ofisi moja
wanafunzi katika shule moja
wanamichezo wa sehemu fulani.
 Misimu ya kitarafa
Misimu ya kitarafa huchukua eneo kubwa/pana kidogo kimatumizi inaweza kutumika hata kwenye tarafa, wilaya, mkoa au kanda. Ueneaji wa misimu hii hutegemea hali au tabia ya muingiliano wa watu katika shughuli za maisha ya kila siku, kama- biashara na michezo, mara kadhaa misimu ya kitarafa hutokana na:
Vitu vilivyo katika eneo fulani
Lugha itumikayo katika eneo fulani
Uzoefu wa mazingira au uwezo wa lugha ya msanii.
 Misimu zagao
Misimu zagao huenea nchi nzima pengine hata kuvuka mipaka ya nchi. Misimu zagao hutumika katika mikoa yote ya nchi na pia hutumika katika vyombo vya habari kama vile magazeti, hutumika pia katika vitabu na vipindi vya redio na television.
Mfano wa misimu zagao ni: -  neno (kabwela), (wakereketwa), (buzi), (bwege) n.k
MATUMIZI /DHIMA ZA MISIMU
Kukuza Lugha
kupamba lugha
Kufanya mawasiliano yawe mafupi na yanayoeleweka kwa haraka
Kuficha lugha ya matusi
Kuwaunganisha watu wa makundi (matabaka) mbalimbali
Kuhifadhi historia ya jamii.
Kuibua hisia mbalimbali za wazungumzaji
Kufurahisha na kuchekesha
Kukosoa na kuiasa jamii
Misimu hupunguza hadhira
MATATIZO YA MISIMU
Misimu huharibu lugha kwa sababu siyo lugha sanifu
Misimu baadhi ya wakati huleta msamiati yenye matusi
Misimu ni lugha ya mafumbo na hufahamika na kikundi kidogo kinachotumia misimu hiyo.
Misimu imetiwa chumvi nyingi kwa hivyo haiaminiki katika jamii
Misimu huzuka na kutoweka
Misimu ina maana nyingi